Watanzania 10 kupewa mafunzo kuhusu gesi ya Helium


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasili Nairobi, Kenya kuhudhuria Mkutano wa Mkuu wa Sita wa Wakuu wa Nchi wa TICAD (TICAD VI) utakaofanyika Agosti 27 -28, mwaka huu. kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli.

Leo asubuhi (Ijumaa, Agosti 26, 2016) Waziri Mkuu amekutana na viongozi wakuu mbalimbali wa makampuni ya kibiashara kutoka Japan ambao wamekuja kuhudhuria mkutano huo.
Waziri Mkuu amekutana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Chiyoda Corporation, Bw. Tadashi Izawa ambapo katika mazungumzo yao, pamoja na kuangalia fursa nyingine katika sekta ya gesi Tanzania, kampuni hiyo imekubali kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa wataalamu kwa sekta ya gesi hususan usindikaji wa gesi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi (Liquefied Natural Gas).
Bw. Izawa amemweleza Waziri Mkuu kwamba wamefurahiswa na taarifa za ugunduzi wa gesi ya Helium hapa nchini Tanzania na kwamba kampuni yake ina teknolojia na uzoefu wa muda mrefu katika kutekeleza miradi ya gesi (Gas value Chain Planning and Execution).
“Tunao uzoefu wa muda mrefu, pia tunazo teknolojia za kuendeleza sekta ya gesi ikiwemo Helium kwa mfano ujuzi wa kutenganisha gesi asilia na helium (Separation of Natural Gas and Helium). Tumetekeleza miradi ya namna hii nchini Qatar ambayo kwa sasa ni ya pili kwa uzalishaji wa gesi hiyo duniani ikitanguliwa na Marekani,” amesema.
Amesema mafunzo hayo yatafanyika kuanzia mwakani na yatalenga vijana wasiopungua 10 kutoka Tanzania ambao wamehitimu shahada za uhandisi kwani wameshafanya hivyo kwa vijana wanane kutoka Msumbiji.
Waziri Mkuu alimshukuru Vw. Izawa kwa mpango wao wa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania lakini akamtaka pia waangalie uwezekano wa kuwasaidia vijana wanaotoka maeneo husika yenye gesi ili wapatiwe mafunzo ambayo yatawawezesha kumudu baadhi ya kazi kwenye viwanda vya kusindika gesi. CHANZO EATV

Post a Comment

Hakuna maoni